Historia Kamili Ya Baraza Kuu La Waislamu Tanzania
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), linaadhimisha miaka 56 tangu lilipoanzishwa mwaka 1968. Bila shaka Watanzania wengi hawaifahamu historia kamili ya kuanzishwa kwake kulitokana na watu gani, walikutana vipi na nini kiliwasukuma kuanzisha chombo hicho. Mzee Omar Nzowa ambaye ni mmoja wa waasisi wa Bakwata anaeleza ni kwa jinsi gani Waislamu walifikia kuanzisha chombo hicho na hatua mbalimbali walizopitia kabla ya kuwapo kwa baraza hilo.
Kabla ya kuanzishwa kwa Bakwata. Mzee Nzowa anasema kabla ya Tanganyika kupata uhuru, jamii za Waislamu katika mikoa mbalimbali nchini zilikuwa na umoja ulioundwa kuanzia ngazi za misikiti hadi wilaya. Anasema umoja ni sehemu ya mafundisho ya dini hiyo, hivyo kabla ya kuwa na chombo chochote kilichokuwa kikiwaunganisha katika kundi kubwa, Waislamu walikuwa wakikutana kupitia misikiti kuanzia kwenye vijiji.
“Baadaye ilionekana kuna haja ya kuunda umoja au jumuiya ngazi ya wilaya. Kwa mfano kule kwetu tuliunda Iringa Muslim Association, Dar es Salaam wakaanzisha yao, Tanga, Bukoba na maeneo mengine vilianzishwa vyama kama hivyo.” “Vyama au jumuiya hizi zilikuwa na lengo kuu la kuwaweka pamoja Waislamu, kujadili mambo mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa jamii. Wakati huo huo kupitia vyama hivyo harakati za kujipatia uhuru na kutaka kujitawala zilikuwa zikiendelea,” anasema Mzee Nzowa aliyezaliwa mwaka 1934 na kuwa Katibu wa Iringa Muslim Association”
Anasema baadaye alikuja kiongozi wa Waislamu wa madhehebu ya Ismailiya, Agha Khan aliyeshauri kuanzishwa kwa Jumuiya ya Waislamu Afrika Mashariki (East African Muslim Welfare Society) ili kuwaunganisha Waislamu wa Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa mujibu wa Mzee Nzowa, pendekezo hilo liliungwa mkono na jumuiya au vyama mbalimbali vya Waislamu vilivyoko wilayani na baadaye ulianzishwa umoja huo. Anasema mbali na kuwaunganisha Waislamu, ilielezwa kuwa Agha Khan alidhamiria kuwasaidia kwa namna mbalimbali wanachama wa jumuiya hiyo iliyokuwa ikiiunganisha Afrika Mashariki.
Misaada hiyo ililenga sekta ya elimu, uchumi na ustawi wa jamii ambapo Agha Khan alisaidia ujenzi wa misikiti na shule zilizomilikiwa na Waislamu. “Sehemu mbalimbali walifaidika na misaada hiyo ambayo hata hivyo ilikuwa na sharti la kuchangia asilimia 50 ya gharama zilizohitajika kukamilisha ujenzi husika,” anasema.
Kujiondoa East Africa Muslim Welfare Society
Anasema baada ya uhuru wa Tanganyika na baadaye, Watanzania walikuwa huru kupaza sauti. Waislamu nao wakaanza kuhoji kuhusu jumuiya hiyo. Moja ya maeneo waliyokuwa wakihoji ni kama wanaongozwa na watu wenye elimu ya kutosha katika masuala ya dini. “Viongozi tukaanza kuwekwa kitimoto kila unakopita Waislamu wanahoji. Awali ilianza chinichini baadaye sauti zikaanza kupazwa. Ilifikia wakati tukaona ipo haja ya kujadili kuhusu jambo hili kwa mapana zaidi.
Anasema kwa kumbukumbu zake vuguvugu la Waislamu kutaka kujitoa katika jumuiya hiyo lilianza mwaka 1963 kabla ya vyama wanachama wa jumuiya hiyo nchini kuanza kujiondoa. Anasema hali ilipofikia hapo walilazimika kuitisha mkutano wa kujadili ambapo yaliibuka makundi mawili moja likiunga mkono kuendelea kuwa katika umoja huo na lingine likipinga. Mzee Nzowa anasema walikubaliana kurudi kwa Waislamu mikoani kupata maoni yao juu ya hatua hiyo ili sauti ya wengi uwe uamuzi wa mwisho.
“Ilikuwa ni kama kampeni vile! Kundi lililokuwa likitetea kuendelea kuwa wanachama wa Jumuiya ya Waislamu Afrika Mashariki na lile lililotaka tujiondoe, wote walipita kwa Waislamu kueleza kwa undani kuhusu jambo hilo kisha kusikiliza wanasemaje. “Mwisho sauti za wengi zilitaka tujiondoe na hapo mlango ukafunguliwa rasmi kutoka katika jumuiya hiyo, ingawa baadhi ya mikoa mapema kabla ya hapo ilishatangaza kujiondoa ikianza Tanga, Bukoba (Kagera) na Iringa tulikuwa watatu kujiondoa,” anasema.
Mkutano wa uamuzi, kuzaliwa Bakwata
Anasema Desemba mwaka 1968, ulifanyika mkutano mkubwa uliokuwa na uwakilishi wa Waislamu kutoka kila mkoa wa Tanzania Bara na Zanzibar ambao kwa kauli moja uliridhia kujiondoa rasmi katika jumuiya hiyo. Mzee Nzowa anasema Waislamu walikutana kwa siku mbili katika ukumbi wa Mkwawa mkoani Iringa ambapo walijadiili na kukubaliana kujiondoa East Africa Muslim Welfare Society na kuanzisha Bakwata. “Lengo la kuanzisha Bakwata na sababu ya kujiondoa katika jumuiya ile vilikuwa wazi…Tulitaka kuwa na viongozi wanataaluma wa dini, watakaoweza kuisaidia jamii ya Waislamu sio kujiongoza katika mambo ya kijamii tu bali hata kupata majibu sahihi ya masuala ya kidini yanapojitokeza,” anasema.
Je Serikali ilitoa msukumo
Mzee Nzowa anasema umoja wa Waislamu unatokana na maagizo yaliyomo katika kitabu chao kitakatifu cha Qur’an na kwamba walilitambua hilo kwa muda mrefu, ndio maana walikuwa na vyama au jumuiya zao katika ngazi za wilaya, hivyo hakuna aliyewasukuma kuendeleza harakati za kujiimarisha katika umoja wao. Anasema Serikali haikuchagiza kwa namna yoyote kuanzishwa kwa Bakwata, bali ulikuwa utashi wa Waislamu wenyewe kuona kwanza wanatumia vyema haki yao ya kuwa na kiongozi wanayemwona anafaa kuwaongoza katika masuala ya dini na kuhakikisha uislamu unakuwa katika mikono salama ya watu watakaoongoza vyema bila kuchanganya maslahi mengine.
“Binafsi nimeshiriki katika harakati zote za kidini kuanzia kule kwenye jumuiya ngazi ya msikiti, wilaya, ilipokuja Jumuiya ya Waislamu ya Afrika Mashariki mpaka tunaanzisha baraza hili. Hakuna popote alipokuja kiongozi wa Serikali kushinikiza kuundwa kwa chombo hiki. “Upo upotoshaji unafanywa na baadhi ya watu tena kwa bahati mbaya baadhi yao pengine walikuwa hawajazaliwa wakati harakati hizi zikifanyika, hawana uelewa sahihi kuanzia vuguvugu mpaka kuanzishwa kwa baraza hili. Ni vyema wakakaa wakasikiliza na kufuatilia historia sahihi ya Bakwata kabla ya kutoa mihadhara au kuchapisha maandiko,” anasema.
Anasema imekuwa ikipotoshwa hata asili ya jina la Bakwata, lakini ukweli ni kwamba lilitokana na mkutano wa Iringa ambako lilipitishwa baada ya kupendekezwa majina kadhaa.
HijjaJamiiMaarifaMafundishoMaishaMaleziMatibabuMatukioQuranSunnah
Leave a comment