Vitu 10 Unavyokosa Endapo Haujui Kusoma Quran Tukufu

By / 1 year ago / Jamii / 1 Comment
Vitu 10 Unavyokosa Endapo Haujui Kusoma Quran Tukufu

Zifuatazo ni baadhi ya fadhila zilizotajwa katika Hadiyth za Mtume Muhammad (S.A.W), za kusoma na kuhifadhi Qur-aan tukufu.

1. Aliye Bora Kabisa Ni Ambaye Anajifunza Na Kuifundisha Qur-aan:

Imepokelewa kutoka kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mbora wenu ni yule mwenye kujifunza Qur-aan kisha akaifundisha)) [Al-Bukhaariy]

2. Anayeisoma Kwa Mashaka Hupata Thawabu Mara Mbili:

Imepokelewa kutoka kwa ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yule aliyekuwa hodari wa kusoma Qur-aan atakuwa pamoja na Malaika Wajumbe, watukufu watiifu. Na yule ambaye anaisoma Qur-aan na anaikariri mara kwa mara huku anaona ugumu mkubwa, atapata ujira mara mbili)). [Al-Bukhaariy na Muslim]

Imekusudiwa ni mtu mwenye ulimi mzito au ambaye ndio kwanza anaanza kujifunza na hupata shida kuisoma, lakini inampasa Muislamu ajitahidi kujifunza kuisoma kisawasawa ipasavyo.

3. Watu Wanaoshikamana Na Qur-aan Ni Watu Bora Kabisa Mbele Ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

Imepokelewa kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Anao watu wake kati ya wanaadam)). Wakamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah ni nani hao? Akasema: ((Hao ni watu wa Qur-aan na ni watu wa Allaah na wateule Wake)) [Ahmad, Ibn Maajah]

4. Mfano Wa Anayeisoma Qur-aan Ni Harufu Na Ladha Nzuri, Kinyume Na Asiyeisoma:

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Muwsaa Al-Ash’ariyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Mfano wa Muumini ambaye anayesoma Qur-aan ni kama tunda la Utrujjah; harufu yake nzuri na ladha yake nzuri. Na mfano wa Muumini asiyesoma Qur-aan mfano wake kama tende zisizokuwa na harufu lakini zina ladha tamu)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Utrujjah: Ni tunda linalofanana na ndimu yenye rangi ya chungwa inayokaribia rangi ya dhahabu. Tunda hilo linajulikana kama tufaha la ki-Ajemi, lina harufu nzuri.

5. Anayeisoma Qur-aan Hupata Thawabu Kwa Kila Herufi Anayoitamka:

Imepokelewa kutoka kwa Ibn Mas‘uwd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayesoma herufi moja katika Kitabu cha Allaah atapata hasanah (jema) moja, na kila hasanah moja ni sawa na thawabu kumi, wala sisemi ‘Alif-Laam-Miym‘ ni herufi moja, bali Alif ni herufi moja na Laam ni herufi moja na Miym ni herufi moja)) [At-Tirimidhiy na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy (2910), Swahiyh Al-Jaami’ (6469), As-Silsilah Asw-Swahiyhah (3327)]

Mfano wa idadi za thawabu hizo za kuisoma kwa kila herufi ni kuisoma, بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Bismillahir-Rahmaanir-Rahiym, yenye herufi 19, hivyo 19 x 10 ni sawa na thawabu 190.

Suwrah ya mwisho kabisa katika Qur-aan ambayo ni Suwratun-Naas [Qur-aan 114] ) ina herufi 80. Kwa hivyo basi, hesabu ya thawabu zake ni  80 x 10 ni sawa na thawabu 800.  Na thawabu hizo utazichuma kwa chini ya dakika moja!  Seuze basi pindi utakaposoma ukurasa mmoja wa Qur-aan? Au Suwrah nzima ya Qur-aan? Au Juzuu nzima? Au je, thawabu ngapi utazichuma pindi ukikhitimisha kuisoma Qur-aan kila mwezi?

6. Anayeisoma Qur-aan Itakuwa Ni Shafaa’ah (Kiombezi) Siku Ya Qiyaamah:

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba: Nimemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Someni Qur-aan kwani itakuja siku ya Qiyaamah kuwa ni Shafaa’ah kwa swahibu yake [mwenye kuisoma]) [Muslim]

7. Qur-aan Humnyanyua Mtu Daraja Ya Juu Na Humdhalilisha Asiyeandamana Nayo:

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Ama hakika Nabiy wenu amesema: ((Allaah Atawanyanyua baadhi ya watu kwa Kitabu hiki (Qur-aan) na Atawadhalilisha wengine kwa kitabu hiki)) [Muslim]

8. Mwenye Kuihifadhi Qur-aan Na Kuifanyia Kazi Atapandishwa Daraja Za Jannah: 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Huambiwa Swahibu wa Qur-aan: “Soma na panda juu (daraja za Jannah) na uisome kwa Tartiyl (ipasavyo kwa hukmu za Tajwiyd) kama ulivyokuwa ukiisoma ulipokuwa duniani, kwani makazi yako ni pale utakapofika katika Aayah ya mwisho utakayoisoma”)). [At-Tirmidhiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh At-Tirmidhiy na Swahiyh Al-Jaami’]

Wengi kati ya ‘Ulamaa wamesema kuwa aliyekusudiwa kuwa ni “Swaahibul-Qur-aan” ni mwenye kuihifadhi na kuifanyia kazi wala si kuihifadhi bila ya kuifanyia kazi au kuisoma bila ya kuhifadhi.

Na Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu-Allaah) amesema: “Tambua kwamba iliyokusudiwa kuhusu “Swahibu wa Qur-aan” ni mwenye kuihifadhi moyoni… [Silsilah Al-Ahaadiyth Asw-Swahiyhah (5/284)

Na amesema Ibn Hajar Al-Haytamiy (Rahimahu-Allaah): “Khabari iliyotajwa ni makhsusi kwa anayeihifadhi moyoni si kwa anayeisoma tu…” [Al-Haytamiy, uk. 113]

9. Wanaosoma Na Kujifunza Qur-aan, Huteremka Malaika Wa M/Mungu Na Kuwazunguka Kwa Utulivu Na Rahmah

Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hawakusanyiki pamoja watu katika nyumba miongoni mwa nyumba za Allaah wakisoma Kitabu cha Allaah, na wanafundishana baina yao, ila huwateremkia utulivu na hufunikwa na Rahmah na Malaika huwazunguka na Allaah Anawataja mbele ya [Malaika] aliokuwa nao)) [Muslim Abuu Daawuwd, Ibn Maajah, Ahmad]. Pia…

Amesimulia Usayd bin Khudhwayr (رضي الله عنه) kwamba alipokuwa akisoma akiwa katika mirbad yake, farasi wake alishtuka. Akasoma, akashtuka tena, akasoma akashtuka tena. Akasema Usayd: Nikaogopa asije kumkanyaga Yahyaa (mwanawe). Nikainuka kumwendea (farasi) nikaona kitu kama kivuli juu ya kichwa changu kama kina kandili kikipanda mbinguni hadi kikapotea. Nikamwendea Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) asubuhi yake nikamwambia: Ee Rasuli wa Allaah, jana usiku nilipokuwa katika mirbad yangu nikisoma Qur-aan, farasi wangu alishtuka! Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ungeliendelea kusoma Ibn Khudhwayr.” Akasema: Nilisoma lakini alishtuka tena. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ungeliendelea kusoma Ibn Khudhwayr.” Akasema: Nilisoma lakini alishtuka tena. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Ungeliendelea kusoma Ibn Khudhwayr.” Akasema niliondoka kwani Yahyaa alikuwa karibu naye, nikakhofu asimkanyage. Nikaona kama kivuli kikiwa na taa kinapanda juu hadi kikapotea. Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: “Hao ni Malaika walikuwa wakikusikiliza, lau ungeliendelea kusoma hadi asubuhi, watu wangeliwaona wazi wazi bila pazia.” [Al-Bukhaariy, Muslim]

Mirbad – Makazi ya mifugo ya farasi au ngamia.

10. Kuhifadhi Na Kujifunza Maana Ya Qur-aan Ni Bora Kuliko Mapambo Ya Dunia?

Imepokelewa toka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhwiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitujia wakati tulikuwa katika Swuffah akauliza: ((Kuna yeyote miongoni mwenu anayetaka kwenda  soko la Butw-haan au [soko] la Al-‘Aqiyq na akapata humo ngamia wawili wakubwa na walionona bila ya kutenda dhambi au kukata undugu?)) Tukajibu kwamba sote tunapenda kufanya na kupata hivyo. Kisha akasema: ((Basi aende mmoja wenu Masjid akajifunze au asome Aayah mbili katika Kitabu cha Allaah (‘Azza wa Jalla), pindi akifanya hivyo, basi ni bora kuliko ngamia wawili. Na Aayah tatu ni bora kuliko ngamia watatu, na Aayah nne ni bora kuliko ngamia wanne, na mfano wa hivyo hivyo wa Aayah kwa ngamia)) [Muslim, Abuu Daawuwd, Ahmad]

Swuffah: Sehemu katika Masjid Ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliyokuwa wakikaa Maswahaba ambao hali zao walikuwa ni masikini.

Butw-haan: Bonde lilioko kusini mwa mji wa Madiynah kuelekea upande wa Magharibi karibu na Jabali la Sal’. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha katika bonde hilo siku ya vita vya Khandaq

Al-‘Aqiyq: Bonde maarufu kabisa katika mji wa Madiynah au eneo la Al-Hijaaz yote, liko umbali wa maili kilometa mia Kusini na linaelekea  upande wa Mashariki, linajulikana kuwa ni ‘Bonde lililobarikiwa’.

admin

The author didn't add any Information to his profile yet.

One Comment

  • admin16. May, 2024

    Mashallah, Hakika haya mambo kumi ni ya msingi sana kuyajua.

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked. *