Tuendelee Kudumisha Amani Tunaposherehekea Sikukuu Ya Eid
Tuendelee Kudumisha Amani Tunaposherehekea Eid
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasihi waislam nchini waendelee kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano, kuhurumiana, utulivu sambamba na kujiepusha na vitendo vinavyoashiria vurugu, uonevu na uvunjifu wa amani waposherehekea Eid El Adha.
“Tunaposherehekea Eid El Adha ni vema pia tukakumbuka maneno ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam kwamba “Mwenye kufanya maaswi siku ya Eid ni sawa na kumuasi Allah Sub-hanahu Wata’ala siku ya kiyama”.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 10, 2022) kwenye Baraza la Eid El Adha, lililofanyika katika Msikiti wa Mfalme Muhammad wa Sita wa Morocco uliopo Kinondoni, Dar Es Salaam. Ametumia fursa hiyo kuwasisitiza wananchi umuhimu wa kudumisha amani.
Pia, Waziri Mkuu amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anawasihi waislamu na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuonesha upendo, umoja na mshikamano hata baada ya kumalizika kwa masiku kumi bora katika mwaka yanayopatikana kwenye mwezi wa Dhul-Hijja.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema moja ya jambo adhimu katika Eid El Adha ni kuchinja na jambo hilo limethibitika katika Qur’an Tukufu pale Allah Ta’ala aliposema katika surah ya 108 ayah ya pili kwamba basi swali kwa ajili ya Mola wako na chinja kwa ajili yake.
“Hivyo basi, nami nahimiza kwamba tutumie fursa hiyo ya kuchinja kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhila mbalimbali alizotujalia pamoja na kuwahurumia na kuwaonesha upendo wale wenzetu miongoni mwa maskini na mafakiri. Lengo ni kuhakikisha walionacho na wasionacho tunakuwa kitu kimoja na kufurahi pamoja.”
Wakati huo huo, Mheshimiwa Majaliwa amewasisitiza wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika tarehe 23 Agosti 2022. “Tujitokeze kwa wingi kuhesabiwa na kuunga mkono zoezi hilo. Tutoe ushirikiano kwa Makarani wa Sensa na Watendaji wetu wa Mitaa katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022.”
Waziri Mkuu amewapongeza viongozi wote wa dini nchini, vyombo vya habari kwa kuendelea kuelimisha na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa mwaka 2022 linalotarajia kufanyika nchini Agosti 23. “Maendeleo yetu yanatokana na kujua idadi ya watu tulionao tuendelee kuelimisha wananchi kushiriki katika zoezi hilo.”
Pia amempongeza Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally pamoja na Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA), kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuiunga mkono Serikali katika utoaji na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo na elimu na afya.
Kwa upande wake, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally amesema sense ni msingi mkubwa wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, hivyo amewaagiza Masheikh wa mikoa na wilaya waendelee kuwahimisha waislamu kote nchini wajitokeze kuhesabiwa siku hiyo itakapofika.
“Suala la sensa ni jambo muhimu na linakubalika katika sheria za uislamu. Kama hakuna sensa hakuna maendeleo kwa sababu hata nyumbani kwako lazima uwe na sensa kama una watoto 13 utatafuta unga na nyama ya kutosha watoto 13. Jitokezeni kuhesabiwa Serikali inataka kujua idadi ya wananchi wake ili iweze kupanga mipango ya maendeleo na utoaji wa huduma za jamii kwa wananchi wake kama afya, maji, umeme na elimu.”
Features
-
10/10
-
5/10
-
2/10
-
1/10
Summary
Ni jukumu letu sote kuzingatia na kuitunza amani ya nchi yetu, hivyo ni heri kuhakikisha tunasherehekea sikukuu yetu pendwa kwa utaratibu na utulivu.
HijjaJamiiMaarifaMafundishoMaishaMaleziMatibabuMatukioQuranSunnah
admin17. May, 2024
Wafanyakazi wa Arkan TV na uongozi wake tunawatakia Sikukuu njema ya Eid-El-Adha.